Friday, 4 March 2011

Nyutinyuti

Vifo mwavisababisha, mwendeshapo kimaluni,
Mwataka kujishibisha, uhai hamthamini,                                                                                                      Kadiri mkiendesha, tutafika salamini,
Haidhuru kutujali, nyutinyuti endesheni.

Heri kutuchelewesha,tusikakose kazini,
Heri kutukokotesha, tusikakose shuleni,
Heri na kutufikisha, tusifie gurufuni,
Hadhuru kutujali, nyutinyuti endesheni.

Zenu nyoyo safisha,tamaa zenu zikeni,
Ni ya muhimu maisha, hamjali kwa nini?
Hela hizi huisha, sing'ang'anie silani,
Haidhuru kutujali, nyutinyuti endesheni.

Serikali imarisha, usalama gurufuni,
Ushuru huwalipisha, mzindukeni jamani,
Barabara rekebisha, madereva mwasemani?
Haidhuru kutujali, nyutinyuti endesheni.

Jumbe huno nafikisha, wanotembea tarikini,
Wangalifu hakikisha, sijitie mwapuzani,
Kiholela kujifisha, tuepuke abadani,
Haidhuru kutujali, nyutinyuti endesheni.

Mapolisi mnachosha, na vyenu visa ndiani,
Milungula mwajilisha, kwangamiza masikini,
Dau langu nafikisha, si kwingine bandarini,
Haidhuru kutujali, nyutinyuti endesheni.