Friday, 25 February 2011

Sondomti

Wanyonnge wenza amka, wakati umewadia
Tushikane kakaka, kwa sauti kuwambia,
Wajuwe tumerevuka, ujinga metuishia,
Tuwagwenye sondomti, wasiule mti Kenya.

Kama ngazi hutuweka, madaraka kupandia,
Kule juu wanapofika, mashuzi hutwachia,
Mwisho huno tumefika, kuchambika sikizia,
Tuwagwenye sondomti, wasiule mti Kenya.

Mali mengi melimbika,uyahe wakatwachia,
Misitu wameifyeka, mvua ikafifia,
Kwa makonde kulimika, ni muhali twawambia,
Tuwagwenye sondomti, wasiule mti Kenya.

Viwanda vyajengeka, jimbo moja fikiria,
Si matope twawapaka,mzinduko twawatia,
Kotekote twachotaka, ni usawa zingatia,
Tuwagwenye sondomti, wasiule mti Kenya.

Masikwota twateseka, migunda wamebania,
Mabadili twayataka, viongozi kuchangia,
Msitake kusifika, domokaya pulikia,
Tuwagwenye sondomti, wasiule mti Kenya.

Zenu tama mtashika, mbali tukiwatupia,
Mzindukie hakika, mbele sana kwangalia,
Na kuzuri tutafika, haki zetu zingatia,
Tuwagwenye sondomti, wasiule mti Kenya.

Ufukara kuinuka, wananchi huumia,
Siasa mbovu epuka, mambo mawi huchangia,
Uchumi hubomoka, ufisadi kwendelia,
Tuwagwenye sondomti, wasiule mti Kenya.

Ufukara kupunguka, uasi hupungukia,
Uongozi kwimarika, mambo mema huchangia,
Kiuchumi huinuka, fanikio kufikia,
Tuwagwenye sondomti, wasiule mti Kenya.

Bandarini tumefika, yetu nanga twaitia,
Ni umoja tunataka,ukabila tupilia,
Yetu haya kusikika, nchi nzuri tutangia,
Tuwagwenye sondomti, wasiule mti Kenya.

1 comment:

  1. Kazi bora, mada unayoishughulikia ni mwafaka. Siasa nchini Kenya itabadili tu wanyonge watakapo gutuka.

    ReplyDelete